JINSI YA KUJIKOMBOA KIMAISHA KWA VIJANA
Jinsi ya Kujikomboa Kimaisha Kwa Vijana Hapa chini kuna muongozo wa kumfanya kijana afanikiwe kimaisha. UNACHOAMINI Njia ya kwanza ya kijana kujikomboa inaanzia kwenye kile anachoamini katika maisha yake. Katika hali ya kawaida mwanzo wa imani ya mwanadamu hutoka kwa wazazi wake na wakati mwingine mazingira atakayokulia. Kwa mfano, wengi tumekuwa na dini kwa sababu tulizaliwa na wenye dini, kwa maana hiyo hata tunachokiamini hatukuchagua kwa akili zetu wenyewe. Kwa msingi huo, kama kuna walio na dini mbaya (nataja tu), wengi wao wameponzwa na kile walichorithishwa na wazazi wao. Hali iko hivyo kwenye njia hii ya kwanza ya kijana kuelekea kwenye mafanikio. Wengi tumezaliwa na kurithishwa imani ya kutofanikiwa. Wazazi wetu walitulea kwa kutuambia maisha ni magumu, hatuwezi kufanikiwa, sisi ni masikini, duni na maneno kama hayo ya kukatisha tamaa. Hata hivyo, walifika mbali zaidi ya hapo kwa kutuita majina “mbwa, nyani, wajinga, wapumbavu, vichaa na waliolaaniwa. Ushahidi wa hili upo mpaka leo, kuna wazazi wanawaita watoto wao majina ya aina hiyo. Kwa hiyo, tukakua tukiamini kuwa sisi ni watu duni ambao hatuwezi kufanikiwa na kama tukiona mafanikio sehemu yoyote tunakuwa na mawazo kuwa, hiyo ni zawadi ya akina fulani wa ukoo mwingine, lakini siyo sisi. Mawazo ya vijana wengi leo yanaamini kuwa, umasikini ni mzigo mkubwa usiokuwa na ufumbuzi. Kitaalamu mtu anapokuwa na mawazo ya kutokufanikiwa hawezi kufanikiwa kwa sababu mafanikio huhitaji nguvu na nguvu za mwili haziwezi kujitokeza kama hazikuvutwa kufanya kazi. Kwa msingi huo, ili mtu aweze kufanikiwa lazima mawazo yake yakubali kuwa mafanikio ni sehemu ya lazima katika maisha. Jambo hili haliwezi kutokea mpaka kijana mwenyewe aliyelelewa kwenye mawazo ya kushindwa apigane vita na mawazo ya kutofanikiwa na kuyashinda. Njia pekee ya kujikomboa na mawazo mgando ni kufuta na kupuuza kauli zote alizoambiwa na wazazi wake kuhusu maisha magumu na kuanza kuamini kuwa, maendeleo ni yake na kwamba muda unahitajika kuyafikia. Nakushauri kijana mwenzangu kuanzia leo uyakatae mawazo ya kushindwa na kukubali udhaifu wako kwamba huwezi kufanikiwa kwa sababu yoyote ile, sema LAZIMA UFANIKIWE KWA KUWA UWEZO HUO UNAO. UNACHOTENDA Ukiangalia tabia ya maisha ya mwanadamu utagundua kuwa anafahamu mambo mengi sana, lakini hatendi sawa na ufahamu wake. Naamini hata vijana wanajua njia za kufanikiwa, lakini hawazifuati. Binafsi kuwafundisha watu kile wanachokifahamu ni sawa na ujinga. Kamwe siwezi kutumia muda wangu kuwaambia vijana ili waendelee wanahitaji kufanya biashara, kuajiriwa, kujiajiri kulima, kwani kufanya hivyo ni kukosa shabaha ya elimu. Ukitaka kuthibitisha hili zungumza na vijana wanaoishi maisha magumu uone kama hawatakuorodheshea njia zaidi ya 100 za kufanikiwa kimaisha! Kumbe tatizo lao si kujua bali ni kutenda ambako ndiyo njia ya kuelekea kwenye mafanikio. Wewe kama kijana jaribu kukumbuka ni biashara, mradi, kazi gani uliyokwishaiwaza na mpaka leo hujaanza kuifanya kwa sababu ambazo hazifahamiki? Miongoni mwa watu wenye tatizo hili wapo ambao si tu kwamba wana wazo, wana fedha, nguvu bali wana uwezo wa kufanya mambo yakawezekana, lakini wamejikuta hawafanyi yale wanayoyaweza na hivyo kubaki watumwa wa umasikini wakiamini tu kuwa, ipo siku wataanza na kufanikiwa. Tatizo kubwa katika mgando huu wa mawazo ni woga wa kushindwa na ugumu wa kuanzisha jambo. Wanasema waswahili ‘MWANZO MGUMU’ hata hivyo haiwi sababu ya wengi kushindwa kufanya mambo kwa kuhofia kukutana na ugumu. Watu wengi waliofanikiwa duniani ni wale ambao walikuwa tayari kuingia katika hatua hii muhimu ya kutenda yale waliyoyawaza na kuyathibitisha kuwa yatasukuma mbele maisha yao. Wote tunajua mwanzo wa kila kitu ni wazo, lakini mawazo yasiyokuwa na matendo ni upuuzi! Vitu ambavyo vimekuwepo duniani na vitakavyokuwepo baadaye vitatokana na ushirikiano wa hatua hizi mbili yaani KUAMINI NA KUTENDA. Ni wakati wako wa kuamini au kugeuza mawazo yako kuwa vitu halisi. Umewaza sana kujenga nyumba mbona hujaanza kujenga? Unasubiri nini kuanza biashara uliyoifanyia utafiti na ukagundua kuwa itakuingizia kipato. Nani kakuzuia usipange chumba chako na kuanza maisha yako? Amka na uanze kufanya yote uliyoyawaza! UNACHOCHAGUA Katika hali ya kawaida mwanadamu wa kawaida ana mahitaji mengi yanayotoka kwenye vitu vingi pia. Ukihitaji mchumba kwa mfano, itakulazimu hitaji lako likutane na wingi wa wachumba tofauti tofauti. Changamoto utakayokutana nayo wakati utakapokuwa unataka kutenda ulichoamini ni kuchagua. Tambua kuwa chochote utakachotaka duniani hakiko peke yake, ukienda sokoni kununua nyanya, utakutana na mafungu mengi ya bidhaa hiyo kiasi cha kukufanya utumie akili kuchagua fungu moja au mawili unayohitaji. Kuwepo na vitu vingi vya kuchagua kama nilivyosema ni moja kati ya tatizo kubwa linalowafanya vijana wengi washindwe kufanikiwa kimaisha kutokana na kutokuwa makini wakati wa kuchagua. Wapo ambao wameshindwa kuendelea kwa sababu tu walichagua wake wabaya, biashara, fani, kazi, kilimo kibaya na mambo mengine. Inawezekana kabisa pengine hata mambo ambayo yanakuendea kombo leo yametokana na kosa lako la kuchagua. Ushauri wangu ni kwamba kila mtu anayetaka kufanikiwa kimaisha lazima ahakikishe mambo anayoyachagua yawe ni yale aliyoyahakiki kuwa yanafaa. TUNACHOPATA Katika hali ya kawaida hakuna mtu anayetafuta kila siku asipate, hili halina ubishi, labda kinachoweza kuwa tofauti ni kiwango cha kupata.
By: Moses Anney ..2014
Comments
Post a Comment